Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana
alimtembelea mfungwa, Rajabu Maranda anayetumikia kifungo cha miaka 18
gerezani kwa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la mgongo.
Mbali na kumtembelea Maranda, Rais Kikwete
alimjulia hali Mwandishi wa Kituo cha Chanel Ten, Salum Mkambala
aliyelazwa hospitalini hapo kutokana na kupata ajali ya gari mapema wiki
hii eneo la Vigwaza mkoani Pwani akitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro
na kuvunjika mguu na mkono wa kulia.
Wote wawili wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya
Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI), wakiendelea na matibabu
huku afya zao zikielezwa kuimarika kadri siku zinavyozidi kwenda.
Rais Kikwete aliwasili MOI saa 6.40 mchana na
kwenda moja kwa moja wodi D aliyolazwa Mkambala kisha alitoka na kwenda
wodi aliyolazwa Maranda.
Rais Kikwete alipofika ulinzi uliimarishwa na hakuruhusiwa mtu yeyote kuingia ndani ya wodi hiyo.
Maranda ambaye ni Kada wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na aliyekuwa Mweka Hazina wa chama hicho Mkoa wa Kigoma
alifikishwa MOI, Februari 16 mwaka huu kwa matatizo ya mgongo na
kufanyiwa upasuaji. Msemaji wa MOI, Jumaa Almasi alisema hali yake
inaendelea kuimarika siku hadi siku.
Maranda na binamu yake Farijala Hussein kwa pamoja
walipatikana na makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yanakabiliwa ya
kujipatia Sh2.2 bilioni za EPA.
Maranda na wenzake pia wanatumikia kifungo cha
miaka mitatu jela ambayo itakwenda sanjari na kifungo cha awali cha
miaka mitano kutokana na kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa, ambayo
ni kula njama, kughushi nyaraka, kutumia hati bandia na kujipatia kiasi
hicho cha fedha.
Novemba 2012, Maranda kwa mara ya tatu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kurejesha Sh616.4 milioni.
Post a Comment