WATU wasiofahamika wamemuua mwanamke mkazi wa Kijiji cha Idiwili, Kata ya Iyula wilayani Mbozi na kumchuna ngozi ya shingo.
Pamoja na kumchuna ngozi marehemu, wauaji hao pia walinyofoa macho, ulimi na koromeo la marehemu.Baada ya mauaji hayo ya kinyama wauaji hao waliutelekeza porini mwili wa marehemu huyo, Angelina Kameza (26).
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Barakaeli Masaki alisema:
“Tumepokea taarifa ya mauaji hayo ya kinyama lakini bado tunaendelea na upelelezi kujua chanzo chake ni kipi.
“Hatuwezi kuhusisha tukio hilo na imani za ushirikina kama baadhi wanavyosikika ila uchunguzi unafanyika kwa kuwa mwili wa marehemu ulikutwa hauna baadhi ya viungo.
“Lakini uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu alikuwa katika ndoa ya wanawake sita baada ya kuolewa na mwanaume mwenye umri wa miaka 70 aliyezaa naye watoto wawili.
“Kabla ya kuolewa na mzee huyo, enzi za uhai wake aliolewa na mwanamme mwingine aliyefariki dunia katika mazingira yanayofanana na haya kwani naye alinyofolewa baadhi ya viungo vya mwili vikiwamo macho, ulimi na koromeo,” alisema Kamanda Masaki.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa katika vyombo vya dola watakapopata taarifa za wauaji hao.
Post a Comment