Featured

    Featured Posts

Loading...

Chadema wampitisha rasmi mgombea ubunge Chalinze

Mgombea Ubunge wa Chalinze kwa tiketi ya Chadema, Mathayo Torongey akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kutambulishwa. Picha na Michael Jamson 
Na Nuzulack Dausen, Mwananchi
Ni Mathayo Torongey ambaye anatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa vyama vya CCM na CUF.
 Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimempitisha Mathayo Torongey kuwa mgombea rasmi wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chalinze.
Akimtambulisha mgombea huyo kwa Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema alisema Torongey alipitishwa juzi na Sekretariati ya chama kwa niaba ya kamati kuu.
“Kikao cha Sekretariati kilizingatia maoni na ushauri wa wanachama na viongozi wetu wa ngazi za chini, Hivyo kwa kuwa hakukuwa na kipingamizi chochote juu ya agombea, chama kilimpitisha Torongey” alisema Mrema.
Torongey alishinda kura za maoni za chama hicho jimboni Chalinze kwa kupata kura 280 dhidi ya 510 zilizopigwa. Aliwashinda wapinzani wake, Omar Mvambo aliyepata kura 84, Francis Mgasa 61 na Frank Mzoo alijinyakulia kura 23.
Mgombea huyo anatarajia kushindana na Fabian Leonard aliyepitishwa na chama cha CUF pamoja na Ridhiwani Kikwete anayesubiriwa kupitishwa na kamati kuu ya CCM (CC-CCM).
Mshindi wa uchaguzi huo anatarajia kuziba pengo la aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Said Bwanamdogo aliyefariki Januari 22 mwaka huu.
Mrema ambaye pia ameteuliwa kuwa Mkuu wa Operesheni wa Uchaguzi mdogo wa Chalinze, alisema Chadema kina imani kubwa na Torongey kushinda uchaguzi wa jimbo hilo unaotarajia kufanyika Aprili 6.
Alisema uchaguzi wa jimbo hilo ni muhimu sana kwa chama kwa kuwa limeshawahi kuongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 15 bila ya kuwa na maendeleo yoyote.
Mrema alisema Chadema hakitishwi na historia ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuwapitisha baadhi ya watoto wa vigogo katika chaguzi ndogo mbalimbali za ubunge zilizowahi kufanyika nchini kama njia ya kuwarithi wazazi wao.
Alizitaja chaguzi zile za Arumeru Mashariki ambapo CCM kilimpitisha Sioi Sumari kumrithi baba yake marehemu Jeremia Sumari, Kalenga; Godfery Mgimwa kumrithi William Mgimwa, na hatimaye uchaguzi wa Chalinze ambapo mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani anatarajia kuwania.
Naye aliyekuwa mgombea katika kura za maoni katika kinyang’anyiro cha ubunge ndani ya chama hicho, Omari Mvambo alisema aliridhishwa na matokeo na mchakato mzima wa uchaguzi.

“Mchakato mzima wa uchaguzi ulienda vizuri na wagombea wote tuliridhika na matokeo yalikuwa sahihi. Kwa hiyo nimeamua kujidhihirisha kuwa ntampa nguvu mgombea aliyepitishwa kushinda uchaguzi,” alibainisha Mvambo.
-Mwananchi 
author

This post was written by: Author Name

Your description comes here!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

CodeNirvana
© Copyright SINGIDA KWETU
Back To Top