Fuatilia mkasa wa kijana huyu, Anord au baba Anjela, mkazi wa Tandika jijini Dar es Salaam ambaye wiki iliyopita aliwashangaza watu waliokuwa katika baa moja iliyopo Davis Corner jijini Dar baada ya kununua bia na kujipiga nayo kichwani, si kwa kufurahisha watu bali kutaka kujiua.
Tukio hilo lilijiri siku ya Jumanne iliyopita ambapo mwandishi wa habari hizi alifika eneo hilo na kufanya mahojiano na mashuhuda kama ifuatavyo:
“Sijui nisemeje! Unajua sisi tulikuwa hapa baa tunakunywa bia huku tukiendelea na maongezi.
“Ghafla huyu kijana alikuja, akanunua bia lakini akaomba isifunguliwe akisema atainywa hivyohivyo. Baada ya muda tukamwona anaipiga kichwani ile chupa hadi ikampasukia kisha akajichomachoma kichwani na shingoni na vipande vyake mpaka damu zikaanza kumtoka kwa wingi.
“Tulishangaa sana. Tena alikuwa akifanya hivyo huku akilia na kusema amechoshwa na ugumu wa maisha, bora ajichome chupa afe ili akapumzike mbinguni ambako hakuna kazi ngumu wala shamba la kulima,” alisema shuhuda huyo.
Aliendelea kumweka wazi kijana huyo kwamba, wakati akiendelea kulia alilalamikia kitendo cha kufukuzwa kazi na bosi wake bila hatia huku akitoka mkono mtupu.
“Huku damu zikizidi kumtoka kwa wingi, pia alisema alipofika nyumbani kwake kukawa hakuna chakula cha kulisha familia. Mbaya zaidi siku mbili mbele, mwenye nyumba alifika na kumwambia anataka kodi ya nyumba kama hana ahame,” alisema shuhuda huyo.
Shuhuda akaendelea: “Bila kujali maumivu makali huku damu ikimtoka, jamaa akasema hapa Dar hana ndugu ambaye yupo tayari kubeba mzigo wa familia yake na pia hana fedha ya kurudia kijijini kwao sijui wapi huko. Ndipo aliona bora ajimalize kuliko familia yake kumwona hana msaada wowote.”
Ilielezwa kwamba baada ya tukio hilo na damu zikiwa zimemchafua mwili mzima, kijana huyo alikwenda kwa mhudumu wa baa hiyo na kumtaka amuuzie bia nyingine lakini alimkatalia akiamini angeendelea kujichoma.
Baada ya kukataliwa, alikwenda kwenye duka la jirani akanunua soda ambayo pia aliipigisha kichwani na kumpasukia.
Inaelezwa kuwa damu zilizidi kumtoka kwa wingi, hakuna mtu aliyemsogelea.
Shuhuda anasema watu walikusanyika, wengine wakapiga simu Kituo cha Polisi Chang’ombe jijini Dar ambapo walifika na kumchukua kwenye ‘difenda’ hadi Hospitali ya Temeke.
Habari zinasema baada ya matibabu, kijana huyo akiwa na bandeji kichwani alirudi kwenye baa hiyo na kuomba kuuziwa bia nyingine lakini hakupewa huduma zaidi ya wateja kumshangaa.
Uwazi lilijaribu kuzungumza na kijana huyo lakini hakuwa tayari zaidi ya kuporomosha matusi na kuendelea kulalamikia ugumu wa maisha.
CREDIT: GPL
Post a Comment