KIJANA mmoja aliyejulikana kwa jina la Mohammed Musa Yusufu maarufu kama Mwarami, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na sare pamoja na kutapeli watu kwa kuuza fomu feki za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mohammed Musa Yusufu anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukutwa na sare feki za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Mdogo wetu Omari alikuja nyumbani na kutuambia amekutana na mtu
anayehusika na fomu za kujiunga na Polisi na kwamba zinauzwa kwa
shilingi 250,000. Kwa kuwa hakuwa na hela, aliamua kuuza kitanda na
godoro na fedha zingine akaongezewa na mama,” alisema mmoja wa dada wa
kijana aliyetapeliwa, aliyejitambulisha kwa jina la Siwa.Alisema baada ya kupata kiasi hicho, Omari alimfuata mtu huyo akiwa na rafiki yake aitwaye Ali Kassimu ambaye naye alitaka kununua fomu hiyo.
Baada ya kumpatia, walipewa fomu hizo na kuelezwa kuwa walitakiwa kusafiri kuelekea Tanga sehemu iitwayo Kibuku ambako ndiko ilipo kambi yao.
Walipofika huko, waliulizwa kuhusu zilipo fomu za kujiunga, lakini walipowaonyesha, askari waliokuwepo kambini hapo walizibaini kuwa hazikuwa halisi, hivyo vijana hao waliwekwa chini ya ulinzi ili kusubiri taratibu zingine kufuatwa.
“Tuliwekwa ndani, mioyo yetu iliumia mno kwani hatukuwa tukifahamu kwamba fomu zile zilikuwa feki. Walipokuwa wakitupa muda wa kuwasiliana na ndugu zetu huku Dar, tuliwaambia tulitapeliwa na yule mjeda feki hivyo ndugu zetu wafanye juu chini jamaa huyo akamatwe,” alisema Omari.
Ndugu wa kijana huyo walianza kumtafuta tapeli huyo maeneo ya Tabata ambako walielekezwa anapoishi na wakafanikiwa kumtia mikononi.
Awali watu hao walijifanya ni wenye kuhitaji fomu kwa ajili ya kujiunga na jeshi hilo la Kujenga Taifa, ambapo aliwapa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuwapa kitambulisho chake cha jeshi ili kuwatoa hofu.
Ghafla walimgeuka na kumweleza ukweli kuwa yeye ni tapeli aliyemponza ndugu yao anayeshikiliwa na polisi, hivyo alitakiwa kuongozana nao kuelekea kituoni.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo hakukaidi, badala yake aliwaomba ahifadhi mzigo aliokuwa ameushika mkononi ndani kwake ili atoke.
Alipoingia ndani, kumbe alitokea mlango wa nyuma na kutokomea kusikojulikana, kitendo kilichowafanya ndugu hao kumkamata mama yake mzazi na kumpeleka polisi hadi hapo mtoto wake atakapopatikana.
“Kwa bahati nzuri mjomba wake akaanza kumsaka, kesho yake akamkamata na kumleta kituo cha polisi hapa Tabata shule,” alisema dada wa mtapeliwa.
Awali, Mohamed aliwahi kukamatwa kwa kosa la kukutwa na sare nyingi za kijeshi kitu kilichosababisha afungwe jela.
Wakati akiendelea kushikiliwa kituoni hapo, askari huyo feki amefunguliwa jalada lenye namba RB/1365/2014 KUJIPATIA PESA NJIA YA UDANGANYIFU.
Post a Comment